Doa jani la kijivu la mahindi

MUHTASARI: Doa jani la kijivu la mahindi umeibuka kama ugonjwa ulioweka kikwazo kwa mazao ya mahindi nchini Marekani  na kusini mwa Afrika katika miaka 25 iliyopita. Ingawa ulidhaniwa kuwa aina moja ya kuvu, Cercospora zeae-maydis, ukaguzi wa chembechembe umeonyesha kuwa kuvu lingine, C. zeina, hupatikana kwa wingi mashariki mwa Marekani na kusini mwa Afrika. Mbegu za kuvu, zinazoishi katika mabaki ya mazao ya awali, hurushwa na matone ya mvua kwenye majani ya chini ya mmea na kusababisha madoa marefu yanayoungana kwenye mimea isiyohimili na kusababisha baka. Mashina hudhoofika na kuanguka wakati wa mikurupuko ya magonjwa. Ugonjwa unaweza kusimamiwa kwa kuharibu mabaki ya mimea baada ya kuvuna, kilimo cha mzunguko, kwa kutumia aina zinazovumilia ugonjwa zaidi, na, matumizi ya dawa za kuua kuvu ikiwa zitaleta faida kiuchumi.

DALILI MUHIMU

Dalili huonekana kwanza kwenye majani ya chini kama madoa madogo sana yaliyozungukwa na kingo za rangi ya manjano, zinazoonekana vizuri zikishikwa kwenye mwanga. Madoa hupanuka sambamba na mishipa ya jani, kwenye aina za mahindi yasiyohimili ugonjwa huu, madoa huwa rangi ya hudhurungi mpaka kijivu, umbo la kimstatili, na kufikia milimita 70 kwa urefu na milimita 4 kwa upana. Madoa yanaweza kujiunga pamoja juu ya majani na kusababisha baka. Mbegu za kuvu hukua kwenye madoa na majani kuanza kuonekana rangi ya fedha-kijivu.

Maambukizi pia huweza kutokea kwenye ala na mabua, ingawa hayaonekani wazi kama yalivyo katika majani. Maambukizi yanaweza kusababisha miozo ambayo husababisha mimea kuanguka.

USIMAMIZI

Kinga – mambo ya kufanya kabla dalili kuonekana

Mbinu za kitamaduni: Doa jani la kijivu husimamiwa vizuri kwa kutumia aina sugu na kuna idadi ya hybrid ambazo zinapatikana sasa Afrika.

Uchaguzi wa aina za mahindi ya kupanda ni muhimu sana. Hakuna aina ambazo ni sugu kabisa (kinga ya maambukizi), lakini nyingi zinaweza ‘kuhimili’ ambapo madoa kwenye jani ni madogo, ugonjwa huja kuchelewa na athari ni ya chini. Angalia katika makampuni na wauzaji wa mbegu katika eneo lako kama aina hybrid zinazohimili doa jani la kijivu zinapatikana. Ama, zingatia matumizi ya hybrid za kibiashara zilizoboreshwa, ambazo ni lazima kununuliwa kila mwaka. Kwa mfano, utafiti wa hivi karibuni (2014) umeonyesha kuwa ZMS616 ni aina maarufu zaidi na wakulima nchini Zambia kwa sababu inafaa kwa aina mbalimbali ya mazingira, ukame na ni sugu dhidi ya magonjwa. Aina nyingine zinazohimili magonjwa ni SC407 na SC411.

Kama wakulima wadogo wanataka kujaribu aina mpya, badala ya kupanda aina zao za kienyeji ambazo si hybrid, inapendekezwa kwamba wapande vishamba vidogo kwanza, kabla ya kuongeza, kama aina mpya inafaa.

Kama mfumo wa kilimo unaotumika ni wa kupanda mbegu moja kwa moja (no tillage au zero tillage), panda mimea ya jamii ya kunde ili ifunike udongo kabla ya kupanda mahindi, mimea inayofaa ni lablab, velvet bean au sunhemp. Kata huo mkunde tu kabla ya kupanda mahindi kwa kufanya matuta bila kulima ardhi. Wakati wa palizi ya kwanza, panda mkunde ambao ni zao la chakula la muda mfupi kama vile maharagwe, peas, pojo au maharage ya soya kama mmea mseto wa kufunika udongo. Kumbuka kwamba mahindi ya mfululizo na mbinu ya no tillage au reduced tillage yana hatari kubwa kwa kuwa hujenga mazingara mazuri ya kuendeleza ugonjwa, hii ni kwa sababu ya kiasi cha mabaki ya mahindi kinachobaki juu ya udongo.

Baada ya kuvuna, kama hutumii mbinu za no tillage au zero tillage, lima na ufunike mabaki ya mahindi au yakusanye na kuyachoma. Hii ni muhimu sana kwa kuwa mbegu za kuvu zilizo kwenye majani na mabua ya mahindi huwezesha kuvu kuishi kutoka msimu mmoja hadi mwingine.

Udhibiti –  mambo ya kufanya baada ya dalili kuonekana

Mbinu za kitamaduni: Hata kama aina inayohimili ugonjwa inatumika, ni muhimu kutumia upanzi wa mzunguko kila baada ya mwaka mmoja au miwili ya kukuza mahindi, ikiwa jani doa la kijivu limeimarika katika shamba hilo. Kumbuka kwamba jani doa la kijivu hushambulia mahindi peke yake. Mimea mingine katika mzunguko haitaambukizwa.

Mbinu za kikemikali: Ikiwa dawa za kuua kuvu zinapatikana na ni nafuu, nyunyiza tu kabla punga kutoka. Nchini Afrika

Kusini, mchanganyiko wa benzimidazoles na triazoles hutumika, na hivi karibuni strobilurins. Hata hivyo, hizi ni ghali na kuna uwezekano zisiwe na faida kiuchumi isipokuwa kwa mashamba makubwa ya kibiashara.

VISABABISHI

Doa jani la kijivu mara ya kwanza lilidhaniwa kuwa husababishwa na kuvu, Cercospora zeae-maydis. Baadaye, iligunduliwa kwamba kulikuwa na zaidi ya aina moja, kulikuwa na C. sorghi, na makundi mawili ndani ya C. zeae-maydis: Kundi I ndilo linalopatikana kwa wingi Marekani, na hutokea pia mahali pengine, na Kundi II hutokea hasa Marekani na Afrika. Uchunguzi wa chembechembe sasa umegundua kwamba Kundi II ni aina tofauti,

  1. zeina, na kwamba C. zeae-maydis haipatikani nchini Afrika Kusini. Kama C. zeae-maydis inapatikana katika maeneo mengine ya bara la Afrika ni jambo linalohitaji kutatuliwa. Inakisiwa kwamba C. zeina, aina ya Kiafrika, ilikuja kutoka kwa mtama kwa sababu ya vile chembechembe zake zinavyofanana na aina ya kuvu ya mtama C. sorghi.

Doa jani la kijivu ni ugonjwa mbaya wa kuvu wa mahindi. Ulianza kusambaa kwa mara ya kwanza katika miaka ya 1990 mapema. Ukali wa ugonjwa hutegemea mambo matatu: kiasi cha kuvu kinachoishi katika mabaki kutokana na mazao ya awali, kiwango cha kuvumilia/usugu wa aina hiyo ya mahindi na muhimu zaidi, hali ya hewa.

Kuvu linaweza kuishi zaidi ya mwaka kati ya mazao na mabaki ya mahindi yaliyoachwa kwenye shamba. Mbegu za kuvu hurushwa na mvua kwa majani ya chini ya mahindi. Hakuna ushahidi kwamba kuvu huenea kupitia juu au ndani ya mbegu.

Majani ya chini yanapoambukizwa, matone ya mvua hurusha mbegu za kuvu kwa majani ya juu na majani ya mimea jirani. Kuenea mbali zaidi hutokea kupitia mbegu za kuvu zinazobebwa na upepo. Muda kutoka maambukizi na kuzaliwa kwa mbegu za kuvu hutofautiana kutoka siku 15 hadi 30 kutegemea uwezo wa mmea wa kuvumilia ugonjwa. Ugonjwa huu mara nyingi huonekana baada ya vipindi vya siku za joto (nyuzi 25-32) na mawingu na umande mzito.

ATHARI

Ugonjwa huu umekuwa mmoja wa magonjwa makubwa zaidi ya mahindi duniani kote. Huleta wasiwasi sana hasa katika Marekani na Afrika. Nchini Marekani, ugonjwa umeongezeka kwa sababu ya mbinu ya kilimo ya no tillage na mahindi ya hybrid kutoweza kuhimili ugonjwa. Katika baadhi ya majimbo ya Marekani yaliyo katika ukanda wa mahindi, mavuno ya mahindi katika miaka ya 1990 yanasemekana kushuka kwa asilimia 20 hadi 40 kutokana na ugonjwa wa jani doa la kijivu. Barani Afrika, kumekuwa na taarifa za hasara za kiuchumi kutoka Afrika Kusini, lakini bado hazijaelezewa katika Mashariki, Magharibi na Afrika ya Kati ambako pia ugonjwa unapatikana sasa. Athari inategemea wakati majani manane au tisa yaliyo juu ya mmea wa mahindi yanapoambukizwa, na kiasi cha ugonjwa kinachoendelea juu yao, kwa kuwa haya huamua asilimia 70 mpaka 90 ya mavuno: maambukizi yakianza mapema ndivyo hasara ya mavuno inavyozidi. Kama ugonjwa huo haujaathiri majani haya ya juu mpaka wiki 6 baada ya kutoa punga, basi hasara ya mavuno itakuwa ndogo. Hasara ya mazao pia hutegemea muda unaochukua mmea kukomaa. Mahindi ya hybrid nchini Afrika Kusini na nyingine za Afrika hushambuliwa zaidi na ugonjwa huu kwa kuwa huchukua muda mrefu kukomaa, hivyo kupatia kuvu muda zaidi wa kuyaharibu.

UENEAJI

Ugonjwa huu uko Amerika ya Kaskazini na Kusini, Amerika ya Kati na Caribbean, na ueneaji mdogo katika Asia. Katika

Afrika, umeenea sana Ethiopia, Kenya, Malawi, Msumbiji, Afrika Kusini, Swaziland na Zimbabwe. Pia, sasa unapatikana Cameroon, Nigeria na Tanzania, na kimaeneo nchini Uganda na Zambia. Usambazaji wa aina mbili, Cercospora zeaemaydis na C. zeina hutofautiana. Cercospora zeae-maydis inapatikana Amerika ya Kaskazini, Kusini na Kati, Caribbean na Afrika (lakini si Afrika Kusini), C. zeina iko China, Brazil, ukanda wa mahindi wa mashariki ya Amerika na kote barani Afrika.

MASOMO ZAIDI

Cercospora zeae-maydis. CABI Crop Protection Compendium. (http://bit.ly/1UOLzv2).

Crous PW, Groenewald JZ, Groenewald M. Caldwell P, Braun U, Harrington TC (2006) Species of Cercospora associated with grey leaf spot of maize. Studies in Mycology 55:189–197 (http://www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC2104713/).

Stromberg EL (2009) Gray leaf spot disease of corn. Virginia Cooperative Extension. Virginia Tech. (http://bit.ly/1IRTgMd). Wise K (2010) Gray leaf spot. Purdue Extension. (https://www.extension.purdue.edu/extmedia/bp/BP-56-W.pdf).

Leave a Reply