Kilimo cha pilipili HOHO

Ni muhimu kuchagua eneo linalofaa kwa kilimo cha pilipili hoho kabla ya kuanza uzalishaji. Ni vyema eneo litakalotumika katika kilimo cha pilipili hoho liwe na urahisi wa upatikanaji maji kurahisisha umwagiliaji kwa kilimo cha umwagiliaji.

UTANGULIZI

Pilipili hoho kama linavyotambulika kitaalam Capsicum annuum ni zao la mboga mboga lenye asili ya Amerika ya Kusini ambako lilisambaa mpaka sasa kulimwa katika maeneo mengi duniani yenye hali ya hewa tofauti. Hapa Tanzania pilipili hoho hulimwa kwa wingi katika mikoa ya Morogoro (Mgeta, Mlali) Arusha, Iringa, Kilimanjaro na Mbeya. Sehemu nyingine zinazolima pilipili hoho ni Ruvuma na Tabora.  Pilipili hoho huzaa matunda ya rangi tofauti kama vile kijani, nyekundu, njano, machungwa na zambalau. Kwa Tanzania pilipili zinazolimwa kwa wingi ni zile za matunda ya kijani, nyekundu na njano.

 

Matumizi ya Pilipili hoho

Pilipili hoho hutumika kwa matumizi ya nyumbani kama kiungo kuongeza ladha na harufu katika vyakula. Vilevile pilipili hoho hutumika kwa matumizi ya usindikaji viwandani  katika kutengeneza rangi za asili za vyakula na vipodozi ambazo kwa sasa hupendwa zaidi kuliko zile zinazotokana na kemikali.

 

Aina za Pilipili hoho

Kulingana na umbo la tunda kuna aina mbili za pilipili hoho ambazo ni pilipili zilizochongoka na pilipili za duara. Pilipili zilizo chongoka zinanukia sana ukilinganisha na pilipili za duara. Kwa Tanzania pilipili zinazolimwa kwa wingi ni zile zenye umbo la duara kwa sababu ni nene na hivyo zina soko zuri.

pilipili hoho za rangi

 
Pilipili Hoho

Aina za mbegu

Kuna aina tofauti za mbegu za pilipili hoho zinazo patikana Tanzania kama vile Calfornia wonder, Emerald Giant, Sweet Neapotitan, Yolo Wonder, Pimiento na Keystone Resistant Giant.  Mbegu zinazopendelewa na wengi ni;

  • Calfornia wonder huzaa matunda makubwa, matamu yenye umbo la duara na kuta nene.
  • Yolo wonder hustahimili magojwa ya batoto na kuzaa sana matunda ya kijani makubwa ya duara yenye kuta nene.

 

UCHAGUZI WA ENEO

Ni muhimu kuchagua eneo linalofaa kwa kilimo cha pilipili hoho kabla ya kuanza uzalishaji. Ni vyema eneo litakalotumika katika kilimo cha pilipili hoho liwe na urahisi wa upatikanaji maji kurahisisha umwagiliaji kwa kilimo cha umwagiliaji. Vilevile shamba liwe lenye kufikika kwa urahisi ili kufanya wepesi katika kuhudumia shamba na usafirishaji wa mazao kwenda sokoni au kufikiwa kwa urahisi na wanunuzi wanaofuata mazao shambani.

Shamba la pilipili hoho liwe mbali iwezekanavyo kutoka mahali lilipo shamba la tumbaku ili kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa batobato ya tumbaku unaoenezwa na wadudu kama vidukari na nzi weupe. Vile vile shamba ambalo limetumika kwa kilimo cha mazao ya nyanya, viazi na bilinganya  lisitumike katika kilimo cha pilipili hoho mpaka baada ya muda wa misimu minne kwa kuwa  mazao haya ni jamii moja (solanaceous) na pilipili hoho hivyo magonjwa na wadudu wanaoshambulia mazao haya huweza pia kushambulia zao la pilipili hoho.

 

MAHITAJI YA KIIKOLOJIA

Hali ya Hewa na Mwinuko

Pilipili hoho hustawi vizuri katika maeneo ya mwinuko tofauti tofauti hadi mita 2000 kutoka usawa wa bahari yenye mgawanyo mzuri wa mvua kuanzia kiasi cha mm 600 mpaka mm 700 cha mvua kwa mwaka. Mvua inapokuwa nyingi huweza kuathiri utokaji wa maua na kusababisha kuoza kwa matunda. Pilipili hoho hustawi katika maeneo yenye hali joto tofauti kuanzia nyuzi joto za sentigredi 16 mpaka 28 lakini hustawi vizuri zaidi katika maeneo yenye joto la nyuzi za sentigredi 20 mpaka 25. Hali joto chini ya nyuzi za sentigredi 16 kwa masaa 120 (siku tano) mfululizo husababisha kuwa na utengenezaji mdogo wa matunda na matunda yasiyo na mbegu wakati joto zaidi ya nyuzi joto za sentigredi 30 husababisha upotevu wa maji kwa wingi katika mmea.

 

Udongo

Kwa ujumla pilipili hoho hustawi karibu kwenye udongo wa aina zote wenye rutuba, kina na husiotuamisha maji wenye uwezo wa kuifadhi maji vizuri. Udongo wa kichanga uliorutubishwa vizuri hufaa sana katika maeneo yenye hali ya baridi kwa sababu ya kuwa na tabia ya kupata joto kwa urahisi na hivyo kufanya mizizi kukua vizuri katika joto linalostahili. Udongo wenye tindikali nyingi huzorotesha ukuaji wa pilipili hoho hivyo udongo mzuri kwa pilipili hoho ni ule wenye tindikali kati ya Ph 6.0 – 6.8.

 

KUANDAA SHAMBA

Muda wa Kuandaa

Shamba la pilipili hoho liandaliwe mapema mwezi mmoja kabla ya kupandikiza miche shambani kabla ya kuanza kwa mvua za masika. Inashauriwa kuanza maandalizi mapema mwezi Januari kwa kilimo cha kutegemea mvua.

 

Namna ya Kuandaa

Shamba la pilipili hoho huandaliwa kwa kufyeka nyasi, kung’oa visiki na kulima kabla ya kupima na kuweka matuta.

 

Kulima

Shamba hulimwa kwa kutumia jembe la mkono, jembe la kukokotwa na wanyama, power tillers au matrekta. Matumizi ya jembe la kukokotwa na wanyama, power tillers na matrekta hurahisisha shughuli ya kulima na kuifanya iwe na ufanisi kwani hukatua udongo vizuri na kuufanya uwe tifutifu. Unapotumia jembe la mkono katika kulima hakikisha unakatua udongo katika kina cha kutosha sm 20 mpaka sm 30 na kulainisha mabonge. Udongo uliokatuliwa vizuri hupitisha hewa inayohitajika na mmea, hurahisisha ukuaji wa mizizi na kuifadhi maji vizuri.

 

Kupima shamba (field layout)

Ni muhimu kuanza kupima shamba kabla ya kuanza kuandaa matuta ili kupata matuta yaliyo katika mpangilio mzuri na mistari ya mimea shambani iliyonyooka vizuri. Kabla ya kupima matuta ni muhimu pia kujua nafasi ya kupandia utakayo tumia ili kupata ukubwa sahihi wa kila tuta. Kwa mfano kwa nafasi ya kupandia ya sm 60 × sm 40 kwa matuta makubwa unaweza kutengeneza kila tuta katika upana wa sm 1.2 na urefu wowote.  Acha nafasi ya m 1 kuzunguka shamba na njia kila baada ya tuta upana wa sm 50. Tumia Tape measure au kamba yenye vipimo kupima shamba huku ukiweka alama za matuta na njia kwa kuchomeka mambo (pegs) katika kila kona ya tuta na kuzungushia kamba.

 

Kuweka matuta

Inashauliwa kupanda pilipili hoho katika matuta ili kusaidia mizizi kukua vizuri na udongo kuhifadhi maji. Wakati wa kiangazi, tengeneza matuta yaliyodidimia kidogo ili kufanya maji yaweze kukaa kwenye udongo na wakati wa masika matuta yainuliwe kidogo toka kwenye usawa wa ardhi ili kuzuia maji yasituame. Matuta yanaweza kuwa makubwa au madogo kulingana na matakwa ya mkulima. Matuta makubwa hupandwa mistari miwili na matuta madogo hupandwa mstari mmoja. Tengeneza matuta kwa kufuata alama zilizowekwa wakati wa kupima shamba.

 

UPANDAJI

Kitalu

Mbegu za pilipili hoho hupandwa kwa kuanzia kitaluni ambapo miche huoteshwa na kutunzwa kabla ya kupandikizwa shambani. Kitalu inafaa kiandaliwe mapema kabla ya kuanza kwa msimu wa mvua. Hakikisha unafuata taratibu zote za uandaaji na utunzaji wa miche ya mboga kitaluni.

 

Kiasi cha Mbegu

Kiasi cha gramu 1 ya mbegu za pilipili hoho inakadiliwa kuwa na idadi ya mbegu 160 hivyo kiasi cha gramu 100 za mbegu za pilipili hoho kinatosha kupanda eneo la ekari moja ambalo huchukua miche karibu 10,000 hadi 15,000.

 

KUPANDIKIZA

Tabia za miche ya kupandikizwa

Miche ya pilipili hoho inayofaa kupandikizwa shambani ni ile yenye afya ambayo haikuathiriwa na magonjwa wala wadudu yenye kimo cha sm 10 hadi 15 ikiwa na majani halisi matano mpaka sita.

 

Muda wa Kupandikiza

Katika mazingira mazuri miche huwa tayari kwa kupandikizwa baada ya wiki nne tangu kusia. Inapendekezwa kupandikiza miche wakati wa jioni ili iweze kupona kwa urahisi na kuzoea hali ya shambani bila ya kupata mstuko (transplanting shock).

 

Nafasi ya kupandia

Miche ipandikizwe kwa kuzingatia nafasi pendekezwa katika mistari iliyonyooka. Pilipili hoho kutegemeana na aina huweza kupandwa katika nafasi tofauti tofauti sm 60 mpaka sm 75 mstari hadi mstari na sm 30 mpaka sm 45 shimo hadi shimo. Ni muhimu kusoma pakiti ya mbegu husika kujua nafasi pendekezwa kabla ya kuchagua nafasi ya kutumia.

 

Hatua za Kupandikiza

Unaweza kupandikiza miche shambani kwa kufuata hatua zifuatazo;

  1. Mwagia maji mengi shambani na ya kutosha kitaluni masaa kumi na mbili kabla ya kupandikiza ili kulainisha udongo kurahisisha upandikizaji.
  2. Chimba mashimo ya kupandia yenye kimo cha sm 10 katika nafasi iliyopendekezwa kwa mbegu itakayotumika mistari miwili miwili kila tuta kwa kutumia kamba iliyowekwa vipimo.
  3. Weka viganja viwili vya mkono vya samadi iliyoiva katika shimo la kupandia kisha changanya na udongo kupata mchanganyiko mzuri. Kwa mbolea ya kupandia kama DAP weka nusu kizibo cha soda katika kila shimo la kupandia kisha fukia mbolea kwa tabaka dogo la udongo kabla ya kupandikiza mche.
  4. Tifua udongo wa kitalu kwa kunyanyulia kwa kutumia koleo au umma wa shambani bila kuathiri mizizi ya miche ili kung’oa miche yenye udongo kidogo kuzunguka mizizi yake.
  5. Pandikiza miche ikiwa na udongo wake katika mashimo ya kupandia kisha fukia kwa udongo ulio pembeni. Miche ambayo mizizi yake imezungukwa na udongo inapona haraka shambani ukilinganisha na miche ambayo mizizi yake haina udongo. Pandikiza miche ya pilipili hoho katika kina kilekile kama ilivyokuwa kitaluni.
  6. Shindilia udongo kuzunguka mche uliopandikizwa kwa kutumia vidole vya mikono miwili kisha mwagilia maji ya kutosha.

source: https://www.mogriculture.com/2018/02/kilimo-cha-pilipili-hoho-1/

Leave a Reply