KAROTI Mahitaji ya Udongo na hali ya Hewa

Joto

Karoti ni mimea jamii ya “Apiaceace” ambayo hupendelea hali ya baridi kiasi yenye nyuzi joto kati ya 15 oC hadi 20oC. Kwa mavuno bora zaidi, kiwango cha nyuzi joto kati ya 16oC hadi 18oC hufaa zaidi.

Udongo

Zao hili hustawi zaidi katika udongo tifutifu na kichanga, wenye rutuba ya kutosha, wenye kutiririsha maji na kuruhusu mzunguko wa hewa ya kutosha. Udongo bora sharti uwe na kiasi cha kati ya tindikali (Soil pH)

5.5 – 7.0.

Maandalizi ya Shamba

Ili kupata mavuno bora, ni vyema kulima shamba kwa kina kirefu chenye udongo laini. Ni vyema pia shamba liwe na unyevu wa kutosha ili kuwezesha mizizi ya karoti kwenda chini zaidi na kustawi vyema.

 Kilimo cha Matuta

Uzalishaji wa Karoti katika matuta ni muhimu kwa mavuno bora. Matuta husaidia kuboresha mfumo wa hewa katika mizizi na kutiririsha maji. Matuta ya karoti yanapaswa kuwa na kina cha sentimita 30, upana wa mita 1.0 na umbali wa mita 1.5 kati ya tuta na tuta. Matuta haya yanaweza kupandwa mistari mine (4) yenye upana wa sentimita 30 kutoka mstari hadi mstari.

Upandaji wa Karoti

Kiasi cha kilo 1.5 – 6 za mbegu huhitajika kutegemea na nafasi ya kupanda. Upandaji wa kujaza mbegu nyingi hutoa karoti nyingi nyembamba (mimea 500 – 1000 kwa Mita za mraba) na hivyo mbegu nyingi hutumika, na pale karoti nene zinapohitajika (mimea 75 – 120 kwa Mita za mraba), kiasi kidogo cha mbegu huhitajika. Kwa mavuno ya karoti zenye unene wa wastani, kiasi cha mimea 250 kwa mita za mraba hupandwa.

 Hatua

 • Fukua mifereji midogo yenye kina cha sentimita 3 yenye upana wa sentimita 15 – 30 kati ya mstari na mstari na kasha weka mbegu na fukia na udongo kidogo.
 • Weka mbolea iliyooza vizuri ama mboji kwenye mifereji katika mistari.
 • Chanagnya mbegu na vumbi la mbao ili kupunguza uwezekano wa kutumia mbegu nyingi.
 • Nyunyiza mbegu takribani katika mfereji na kisha funika kwa udongo.
 • Ni vizuri kuweka matandazo juu ya tuta kutunza unyevu.
 • Chunguza kama mbegu zimeota na ondoa matandazo ili ziweze kuota na kuapata mwanga wa kutosha.

Kufunikia Mbegu Baada ya kusia

Ni vyema kufunikia mbegu baada ya kusia kwa kutandaza nyasi kavu na laini ili kutunza unyevu na pia kuzuia mvua kuporimosha mbegu pindi inyeshapo kwa wingi. Hali hii pia huboresha kiwango cha utoaji wa mbegu za karoti. Unaweza pia kufunika kwa plastiki  nyeusi kwa siku 3 – 5 kutegemea na hali ya hewa.

Upunguziaji Miche ya karoti

Muda unaofaa kupunguzia karoti ni pale miche inapokuwa na majani 3 au 4 inapokuwa na urefu wa sentimita 5 na kuacha miche katika umbali wa sentimita 5 – 6 (kiasi cha vidole vitatau vya mkono). Upunguziaji wa miche ya karoti na kuacha nafasi sahihi husaidia kupata karoti bora, nene na zilizonyooka. 

Kama miche yote ikiachwa bila kupunguzwa hubanana na hivyo kupata karoti nyembamba na wakati mwingine zilizopinda.

Kagua matuta kila siku mara 3 yaani asubuhi, mchaan na jioni, ondoa plastiki au matandazo mara moja pindi uonapo mmea hata mmoja umeanza kuchomoza ardhini.

 Kuzuia Magugu

Zao la karoti huathiriwa sana na magugu hasa katika mwezi wa kwanza wa uzalishaji, hivyo ni muhimu sana kudhibiti magugu. Njia za kuzuia magugu ni pamoja na kuzingatia palizi mapema na pia unaweza kutumia dawa/viuagugu za kuuwa magugu kwa kuzingatia ushauri wa kitaalamu. 

 Umwagiliaji

Umwagiliaji wa karoti umegawanyika katika awamu mbili. Awamu ya kwanza ni wakati wa kuota ambapo umwagiliaji wa kunyunyiza kwa bomba la mvuke hutumika ili kuhakikisha unyeyu unasambaa vema katika tuta. Mabomba yanapaswa kuwa katika umbali wa mita 6 kutoka bomba moja hadi jingine na pia katika upana wa matuta 5.

Kwa mkulima mdogo, umwagiliaji wa karoti huweza kufanyika kwa mpira au sprinkila ili maji yasambae vizuri. Karoti haihitaji maji yaliyozidi.

Baada ya mbegu kuota, umwagiliaji wa njia ya matone hutumika. Umwagiliaji kwa njia hii una faida nyingi kama vile matumizi kidogo ya maji na kupunguza maambukizi ya magonjwa

 Matumizi ya Mbolea

Ni vizuri kupima udongo ili kujua mahitaji halisi ya mbolea kwani karoti huathirika kwa urahisi pindi kunapokuwa na upungufu au kuzidi kwa kiasi cha rutuba ya mimea hasa Naitrojeni.

Kwa kawaida, matumizi ya mbolea ya naitrojeni huanzia kiasi cha kilo 110 hadi kilo 280 kwa hekta.

Matumizi ya naitrojeni kupita kiasi husababisha kuvunjika kwa mizizi wakati wa kuvuna. Kiwango kidogo cha naitrojeni huweza kuwekwa shamabani kabla ya kupanda, kikichanganywa na mbolea ya phosphate.  Wadudu na Magonjwa

 Wadudu

Funza Weupe (Pyllophaga sp)

Hawa ni wadudu waharibifu sana wa zao la karoti na mazo mengine. Uharibifu unaofanywa na wadudu hawa hupunguza thamani ya mazao na kusababisha hasara kubwa kwa mkulima.

Namna ya Kudhibiti 

 • Zingatia usafi wa shamba wakati wote
 • Chukua sampuli za udongo kabla na wakati wa uzalishaji ili kukagua idadi ya mayai na mabuu. 
 • Tifua na kugeuzageuza udongo ili kuruhusu jua kupenya kwa kipindi cha mwezi mmoja kabla ya kupanda ili kuua wadudu na mayai
 • Tumia viutilifu kulinagan na ushauri wa wataalam.

 Minyoo fundo (Meloydogine sp)

Minyoo aina ya nematode hushambulia sana karoti hasa katika udogo wa kichanga usiokuwa na rutuba ya kutosha. Dalili za mashambulizi ya minyoo hawa ni kuweka nundu nundu kwenye mzizi (karoti)

Dalili hizi hufanana na zile zinazosababishwa na mashambulizi ya wadudu aina ya pythium, hata hivyo tofauti na dalili za pythium, minyoo ya nematode husababisha nundu hata katika ncha ya mizizi ya karoti

Minyoo fundo (Meloydogine sp)

Magonjwa

Ugonjwa wa “ kata kiuno” (damping off)

Ugonjwa huu husababishwa na fangasi (pythim, fusarium Rizoctoria, Verticillum). Ugonjwa huu huathiri idadi ya mimea shambani. Ugonjwa huu hujitokeza sana pale mimea inapokuwa na umri mdogo hasa inapoanza kuota. Mimea hufa kwa kunyauka shina, sentimita chache kutoka ardhini.

Namna ya kudhibiti

 • Ni vema kumwagilia maji kiasi cha wastani.
 • Matunzo bora ya shamba hasa wakati wa palizi
 • Tumia dawa za kuzuia ukungu, soma dawa zilizotajwa kwenye kilimo cha nyanya

Madoa Meusi (Alternaria sp)

 • Ni ugonjwa hatari wa majani. Majani huonekana kama yameungua na wakati mwingine hupukutika kabisa.

 Namna ya Kudhitibi

 • Epuka kutumia maji mengi kupita kiasi
 • Hakikisha shamba lina rutuba ya kutosha
 • Ondoa magugu shambani
 • Tumia dawa za kinga za magonjwa ya ukungu.
 • Epuka kuingia shamba lenye ugonjwa kisha kwenda katika shamba lisilo na ugonjwa ili kuzuia kusambaa kwa vimelea.
 • Fanya kilimo cha mzunguko, usirudie kupanda karoti kwenye eneo moja kwa misimu miwili au mitatu mfululizo.

Ubwiri Unga

Ugonjwa huu huleta madhara zaidi panapokuwa na hali ya ukungu na joto. Dalili za ugonjwa huu ni kuwa na unga unga wa rangi ya kijivu kwenye majani. Ugonjwa huu huweza kuathiri mavuno kwa kiasi kikubwa kwani huzuia mimea kujitengenezea chakula kwa kutumia mionzi ya jua na rangia ya kijani ya majani

Ubwiri unga ( Powdery mildew)

 Kudhibiti

Ubwiri hudhibitiwa kwa mbinu sawa na zile za udhitibi wa madoa meusi hapo juu na kuhusu viuatilifu fuaata maelezo kwenye kijarida cha kilimo cha nyanya.

Kuoza Mizizi (Pythium sp)

Ni ugonjwa wa vimelea vya ukungu unaozeesha mizizi.

Ugonjwa huu pia husababisha mzizi wa karoti kutoa matawi.

Kudhibiti

 • Kama ilivyo ainishwa katika ugonjwa wa “kiuno hapo juu.
 • Epuka kumwagilia maji kupita kiasi hasa katika siku za mwanzo za kupanda
 • Zingatia usafi wa shamba
 • Tumia dawa za kuzuia magonjwa ya ukungu
 • Ng’oa karoti zote ugonjwa na kuchoma masalia yote.

 Matatizo Mengine

Shingo ya Kijani

Tatizo hili hutokea pale sehemu ya juu ya mzizi (karoti inapokuwa wazi pasipo kufunikwa na udongo na hivyo kuchomwa na jua. Ili kukabiliana na tatizo hili. Mkulima anashauriwa kuhakikisha anafukia karoti vyema na udongo zinapokuwa shambani.

 Mizizi kupasuka

Zipo sababu mbalimbali zinazoweza kusababisha tatizo hili. Kati ya sababu hizo ni kuwepo kwa virutubisho vingi kupita kiasi vya naitrojeni katika udongo au kuongezeka ghafla kwa maji katika udongo (mvua nyingi).

Hivyo ni vizuri kubaini hali inayosababisha tatizo kwa wakati huo ili kupanga mkakati wa ufumbuzi.  Uvunaji  mapendekezo Muhimu

 • Vuna wakati udongo ukiwa na unyevu wa kutosha.
 • Tumia Kreti za kuvunia.
 • Chambua kulingana na ubora na ukubwa
 • Hifadhi mavuno yako vizuri kwenye kivuli.
 • Kinga mazao yasiathiriwe na jua na mvua  kuvuna
 • Ng’oa karoti kwa mkono au tumia jembe maalumu la kung’olea
 • Kata majani mara baada ya kuvuna kwa kutumia kisu kikali.

Mwisho 

Muongozo huu, wa kilimo cha nyanya, umeandaliwa na Agronomist Peter (0623642293) na baadhi ya taarifa zimenukuliwa kutoka vyanzo tofautitofauti vya Tanzania Horticulture Association (TAHA)

Leave a Reply