Kilimo cha mboga mboga kutumia chupa za maji

KILIMO CHA MBOGA ZA MAJANI (SPINACH)

Habari mkulima smart! Leo napenda kukuletea somo la kilimo cha mboga za majani (Spinach) kwa kutumia chupa za maji. Kilimo hiki cha mboga za majani ni rafiki kwa mazingira na ni rahisi kufanya ukiwa nyumbani. Aina hii ya kilimo haihitaji eneo kubwa na inaweza kukuingizia kipato iwapo utaifanya kama kilimo biashara.

MAHITAJI

1. Chupa za maji, ujazo wa lita 1.5 au lita 6.
2. Mbegu za spinach.
3. Udongo: tumia udongo unaopatikana chini ya miti yenye kivuli, mara nyingi udongo huu unakuwa mweusi. Ni mzuri sana kwani una mbolea asilia.
4. Chanja ya kubebea chupa

NAMNA YA KULIMA

~ Andaa chupa zako, idadi ya chupa unayotaka. Kwa kuanzia, anza na chupa 60. Zikate chupa zako kama picha inavyoonesha kisha weka udongo kiasi kwenye chupa zako.

~ Otesha mbegu za spinach moja kwa moja kwenye chupa zako kwa vipimo kama inavoonesha picha. Usibananishe sana mbegu.

~ Weka alama ya vijiti pale ulipopandikiza mbegu ili kurahisisha zoezi la umwagiliaji.

~ Panga chupa zako kwenye chanja kama picha inavoonesha kisha iweke chanja sehemu isiyokuwa na jua kali.

UMWAGILIAJI

Mwagilia mbegu za spinach asubuhi na jioni. Zingatia muda wa umwagiliaji ili mbegu zisidhoofike kwa kukosa maji.

UANGALIZI

Mbegu zikianza kuota, mwagilia maji kiasi na ongeza udongo kiasi kuzunguka miche ili kuipa miche ustahimilivu, pia kuipa miche virutubisho muhimu.

~ Endelea kuitunza miche vizuri hadi kufikia ukomavu tayari kwa kuvuna.

KIPATO

Kwa machupa 60, kila chupa linabeba miche mitatu, na wastani kila mche utavuna awamu hadi 4 na kuuza sokoni kwa 400 @awamu.

Hesabu ndogo:

~ 400/ × awamu 4 =1600/@shina

~ 1600/ × miche 180 = 288,000/=

Ukifanya kilimo hiki kwa uaminifu na kwa moyo dhabiti, unaweza kutimiza mahitaji yako madogo madogo au kuanzisha mradi mwingine kwa faida uliyopata.

Karibu kilimo smart; jifunze, elimika, tenda kwa kujiamini. Ishinde hofu na fungua milango ya kipato chako.

4 comments on “Kilimo cha mboga mboga kutumia chupa za maji

    1. Itategemeana na ukubwa wa bustani unayotaka kulima
      Makopo unaweza nunua kuanzia Tsh200 moja kulingana na eneo ulilopo
      Mbegu zinapatikana maduka ya pembejeo bei inategemeana na mahali na ujazo pia

Leave a Reply