MAGONJWA YA KUKU, DALILI NA NAMNA YA KUKABILIANA NAYO

Magonjwa ya kuku yapo mengi. Hata hivyo siyo yote yanatokea mara kwa mara hapa Tanzania. IIi uweze kudhibiti yale yanayotokea katika kundi lako unahitaji kufahamu dalili za jumla za magonjwa hayo…

Unapoigundua moja au zaidi ya dalili za ugonjwa au wadudu chukua hatua mara moja. Yapo magonjwa ambayo yanaweza kuangamiza kundi lote la kuku katika.muda mfupi. Jihadhari na uwezekano wa kupatwa na hasara zinazoletwa na magonjwa ambayo unaweza kuyazuia. Katika sehemu hii utajifunza kwa muhtasari tu dalili za jumla za magonjwa ya kuku na jinsi ya kuyadhibiti.

Dalili za Jumla za Magonjwa ya Kuku.

Kuku kupoteza hamu ya kula.
Kuzubaa na kukaa mahali pamoja kwa muda mrefu (Kutochangamka).
Kushuka kwa kiwango cha utagaji wa mayai.
Vifaranga kutokua upesi au kudumaa. – Macho kuwa na rangi nyekundu.
Kujikunja shingo.
Kutetemeka, kutoa majimaji puani, mdomoni na machoni.
Kutoa mharo (kinyesi) wa rangi ya kijani au wenye mchanganyiko na damu au cheupe.
Ukiona moja au zaidi ya dalili hizi katika kundi lako chukua hatua za kutibu zilizoelezwa hapa chini. Kama hali ni ngumu zaidi omba msaada kwa mtaalam wa tiba ya mifugo ili achunguze mara moja na kukushauri jambo la kufanya.

MAGONJWA MUHIMU YA KUKU NA JINSI YA KUYADHIBITI NA KUTIBU.

Kideri/Mdondo (New Castle Disease)
Picha za kuku wenye kideli

Ugonjwa huu huwapata kuku wakubwa na wadogo na ni miongoni mwa magonjwa hatari ambayo huambukizwa kwa kasi kubwa sana na kusababisha vifo. Ugonjwa huu husababishwa na virusi na huweza kushambulia pia bata, bata mzinga, kanga, kwale na ndege wengineo.

Jinsi unavyoambukiza:

kuku mzima kuvuta hewa yenye virusi vya ugonjwa huu toka kwa kuku mgonjwa.
upepo huweza kuhamisha virusi vya ugonjwa huu toka sehemu hadi sehemu.
watu huweza kuhamisha ugonjwa huu wanapotembea toka sehemu hadi sehemu.
kuku wasio na ugonjwa wakikaa pamoja na kuku wagonjwa.
ndege wanaokula mizoga kama kunguru huweza kusambaza mabaki ya mizoga yenye ugonjwa huu.
Vyombo vya usafiri toka kwenye eneo lenye ugonjwa.
Dalili zake:

Picha ya kuku anayeugua Kideri

homa kali, kuku kuwa dhaifu, kuzubaa na kushusha mabawa na kupoteza hamu ya kula.
kuku kupoteza fahamu na kupooza viungo.
kulegea kwa shingo na inaweza kupinda kuelekea nyuma au pembeni pia huweza kuzungusha shingo.
kuhema kwa shida na hutoa majimaji mdomoni yenye harufu kali.
Kukohoa, kukoroma na kupiga chafya.
Kuharisha kinyesi chenye rangi ya kijani.
Vifo vya mfululizo vinavyoweza kumaliza kuku wote bandani.
Matibabu ya Kideri: Ugonjwa huu unaambukizwa na virusi, hivyo basi hauna tiba, bali kinga.

Kinga ya ugonjwa:

Kuku wasio na ugonjwa wapatiwe chanjo mapema.
Vifaranga wapatiwe chanjo wakiwa na siku tatu (3).
Chanjo irudiwe kila baada ya miezi mitatu
Kuku wagonjwa wauawe na mizoga yao ichomwe moto na kufukiwa.
Hakikisha usafi wa banda la kuku na vyombo vyote wanavyotumia.
Muhimu: Usichanje kuku kama ugonjwa umeshaingia kwenye kundi.

Kuna aina mbili za chanjo ya mdondo.

Chanjo inayoweza kuvumilia joto (Thermostable):

Chanjo hii inaweza kutunzwa katika hali ya joto la kawaida (room temperature) na kuendelea kubaki salama kwa muda wa siku 30. Hutolewa kwa kuku kwa njia ya matone kwenye macho. Kwa kutumia chanjo hii unaweza kuwachanja kuku muda wowote katika siku. Ila inashauriwa kuwa chanja asubuhi ili kupunguza uwezekano wa chanjo kupata miale ya jua ya moja kwa moja.

Chanjo isiyovumilia joto:

Chanjo hii hutunzwa kwenye ubaridi muda wote. Hutolewa kwa kuku kwa kuchanganywa na maji ya kunywa kuku. Ikishachanganywa, huchukua muda mfupi kama wa saa moja na baada ya hapo inaanza kupoteza ubora wake. Kwa hali hiyo, inashauriwa kuwanyima kuku maji kwa muda ili wapate kiu sana na ndipo uwawekee maji ya kunywa yenye chanjo ili wayanywe kwa wingi na kwamuda mfupi. Pia inashauriwa kuwa siku ya chanjo wape kuku chakula kikavu zaidi kabla ili wapate kiu sana.

Muhimu:

Mdondo au kideri ni ugonjwa tishio ambao huweza kuua kuku wote.
Mdondo ukitokea vifo huwa vingi, kuku hupumua kwa taabu, hupooza na wengine huzunguka na kuzungusha kichwa.
Mdondo huweza kuzuiwa kwa chanjo kila baada ya miezi mitatu.
Wafugaji kuku waunde vikundi vya ushirika wa kuchanja mdondo.
Kuhara damu (coccidiosis)
Picha za kuku wenye ugonjwa wa kuhara damu na kinyesi chake.

Maelezo

Ni ugonjwa unaosababishwa na Protozoa ambao hushambulia kuku na wanyama wengine. Ugonjwa huathiri Kuku wadogo na wakubwa.

Jinsi Ugonjwa Unavyoenea

Maambukizi huenea kupitia kinyesi cha kuku wagonjwa kuchafua maji na chakula, udongo na maranda.
Njia kuu ya maambukizi ni kupitia chakula na maji yaliyochafuliwa na vimelea
Maambukizi yanaweza pia kupitia vifaa na vyombo vya shambani, nguo, wadudu na wanyama.
Dalili

Picha ya kuku aliyehara damu

Kuku Kuhara damu
Mbawa kushuka
Kuzubaa na kuacha kutaga
Kukosa hamu ya kula
Kupunguza kasi ya ukuaji na uzito
Kwa kawaida vifo ni vingi
Namna ya kuzuia ugonjwa

Maranda na aina nyingine za malalo yawe makavu wakati wote.
Fuga kuku kwenye mabanda yenye sakafu isiyo na matundu
Vyombo vya chakula na maji visiwekwe chini, vining’inie juu ya sakafu kuzuia kuchafuliwa na kinyesi
Banda lisiwe na msongamano mkubwa wa kuku
Weka utaratibu wa kuhakikisha wafanyakazi , wageni na ndege hawaingii hovyo kwenye shamba/banda
Angamiza mizoga yote kwa njia stahiki kwa kuchoma moto au kufukia kwenye shimo refu ardhini. Pia na
maranda na vifaa vilivyochafuliwa vichomwe.
Kutumia dawa za tiba kwa ajili ya kinga. Hii ifanyike kwa muda mfupi kuepuka kuleta usugu wa vimelea. Lisha vifaranga chakula k i l ichochanganywa na dawa ya kinga coccidiost kama Amprolium au Salfa.
Tiba

Watenge kuku wote Walioambukizwa na wapatie dawa kama Amprolium au salfa au Esb3.

Source https://www.agricpays.com/magonjwa-ya-kuku/

1 comment on “MAGONJWA YA KUKU, DALILI NA NAMNA YA KUKABILIANA NAYO

Leave a Reply