Magonjwa yanayo sumbua kuku na tiba zake part 2.

Ndui ya kuku (Fowl pox)
Picha za kuku wenye ugonjwa wa ndui

Maelezo

Ndui ni ugonjwa unaosababishwa na virusi ambavyo hushambulia zaidi kuku, jamii ya bata na aina nyingi ya ndege pori. Kuku na ndege wa umri tofauti wote huweza kushambuliwa na sehemu zinazoathirika zaidi ni zile zisizo na manyoya. Virusi vinaweza kuishi katika mazingira kwa muda mrefu.

Jinsi Ugonjwa Unavyoenea.

Chanzo cha maambukizi ni vifaa/vyombo vya shambani vilivyochafuliwa na kinyesi cha kuku wagonjwa na wenye vimelea.
Maambukizi pia kuenea kupitia wadudu wanaouma kama chawa, kupe, nzi weusi na mbu.
Maambukizi pia kuenea kupitia majeraha wanayoyapata kuku wanapopigana na kukwaruzana au kugusana
Maambukizi kupitia mfumo wa hewa na chakula.
Dalili

Kuku aliyevimba macho

Ugonjwa unapoathiri ngozi hutokea vidutu vikubwa vya rangi ya kijivu au kahawia kwenye upanga, undu, macho na mdomoni
Ugonjwa unapoathiri sehemu laini za mwili, mabaka madogo meupe hutokea kwenye kona za mdomo, kuzunguka ulimi, ndani ya mdomo na kwenye koo.
Malengelenge kwenye kishungi na kope za macho na sehemu zisizo na manyoya.
Namna ya kuzuia ugonjwa na tiba

Kuchanja kuku wote wakiwa na umri wa miezi miwili.
Watenge kuku wote walioambukizwa na wapewe antibiotic kama OTC plus au salfa pamoja na kusfisha vidonda kwa maji ya chumvi.
Mafua ya kuku (Fowl coryza).
Picha ya kuku mwenye ugonjwa wa fowl coryza.

Maelezo

Huu ni ugonjwa unaosababishwa na bacteria ambao hushambulia zaidi kuku na ndege wa porini. Ugonjwa

hushambulia kuku wa umri wowote.

Jinsi Ugonjwa Unavyoenea

Chanzo cha maambukizi ni maji na chakula kilichochafuliwa na kinyesi cha kuku wagonjwa.
Kuku au ndege wagonjwa huambukiza wenzao kupitia mfumo wa hewa wanapopiga chafya.
Dalili

Ugonjwa huu hushambulia zaidi mfumo wa hewa na hivyo kusababisha dalili zifuatazo:

Makamasi mazito yenye usaha hutoka puani.
Kuku anashindwa kupumua, hukohoa na kupiga chafya.
Harufu mbaya kutoka kinywani na machoni.
Uso mzima unavimba pamoja na upanga.
Namna ya kuzuia na tiba

Usafi wa banda
Kuchanja kuku wote Kabla hawajaambukizwa kama ni tatizo sugu katika eneo
Watibu wanaougua kwa kutumia anti biotic kama sulphamethazine, streptomycine na vitamin.
Kuharisha Kinyesi Cheupe (Bacillary White Diarrhea)
Maelezo

Huu ni ugonjwa wa kuku unaosababishwa na bakteria na hushambulia zaidi kuku wadogo wenye umri hadi wiki tatu. Ugonjwa pia hushambulia aina zote za bata, kanga na ndege wa porini (mbuni).

Jinsi Ugonjwa Unavyoenea

Chanzo cha maambukizi ni maji na chakula kilichochafuliwa na kinyesi cha kuku wagonjwa. Panya, ndege na wanyama wengine wanaweza kueneza ugonjwa kwa kubeba mizoga ya kuku iliyokufa kwa ugonjwa na kuchafua maji na vyakula.
Kuku waliopona baada ya matibabu wanaweza kuendelea kuchafua mazingira na kuwa chanzo cha maambukizi, hivyo waondolewe shambani.
Maambukizi pia yanaweza kupitia katika mayai yanayototolewa na vifaranga kuathirika.
Tahadhari: Wageni na wafanyakazi wanaweza kusambaza ugonjwa kutoka shamba hadi shamba au banda hadi banda.
Vituo vya kutotolea vifaranga vinaweza kuwa chanzo. Hakikisha vifaranga wako hawatoki kwenye kituo chenye kuku wagonjwa.
Dalili

Vifaranga hufa ghafla
Vifaranga wanatotolewa wakiwa wamekufa au dhaifu
Uharo wa rangi nyeupe kama chaki
Hupumua kwa shida
Uharo huganda kwenye manyoya ya sehemu ya kutolea haja
Vifaranga wanapiga sana kelele
Vifaranga wanaonyesha ulemavu Kuvimba magoti
Kuzuia na Kinga pamoja na tiba.

Hakikisha kwamba vifaranga wako wanatoka katika vyanzo vilivyothibitishwa kuwa havina huu ugonjwa
Tengeneza utaratibu wa kufanya usafi wa mabanda na mazingira mara kwa mara unapobadilisha makundi ya kuku kwa kutumia viuatilifu vilivyopendekezwa.
Panga utaratibu wa kuchunguza afya za kuku wote wenye umri zaidi ya miezi mitano (5) mpaka hapo kundi lote litakapoonyesha kwamba hakuna kuku mwenye maambukizi, kuku salama wahamishiwe katika mabanda safi.
Weka utaratibu wa kuhakikisha watu, wanyama, ndege wa aina nyingine na ndege wa porini hawazururi shambani au bandani.
Watenge kuku wagonjwaTumia dawa kama Furazolidone au Sulfadimidine auHata vitunguu saumu menya robo kilo utwange nu kuchanganya na maji lita moja. Chuja uwapatie maji haya kwa muda wa wiki moja.
Kipindupindu cha Kuku (Fowl Cholera)
Maelezo

Ni ugonjwa wa kuku unaosababishwa na bacteria ambao huenea kwa haraka na kusababisha vifo vingi. Ugonjwa hushambulia kuku na ndege wa aina zote ijapokuwa jamii ya bata huathirika zaidi kuliko kuku.

Jinsi Ugonjwa Unavyoenea

Chanzo cha maambukizi ni hewa, maji na chakula kilichochafuliwa na kinyesi cha kuku wagonjwa.
Kwa kawaida ugonjwa huanza kwa kuingiza katika shamba/banda kuku wagonjwa kutoka nje. Baada ya vimelea kuingia huenea kwa kupitia maji au vyakula vilivyochafuliwa.
Udongo uliochafuliwa na kinyesi cha kuku mgonjwa huweza kuchafua maji na vyakula
Hewa kutoka kwa kuku wagonjwa inaweza kuwa chanzo cha maambukizi.
Panya, ndege na wanyama wengine wanaweza kueneza ugonjwa kwa kubeba mizoga ya kuku waliokufa kwa ugonjwa na kuchafua maji na vyakula.
Tahadhari: Wageni na wafanyakazi wanaweza kusambaza ugonjwa kutoka shamba hadi shamba au banda hadi banda.

Dalili

Kuku wanaweza wasionyeshe dalili zozote za ugonjwa, lakini dalili zifuatazo zinaweza kuonekana:

Vifo vya ghafla vya idadi kubwa ya kuku waliokuwa na afya
Kuku wanakonda
Kuku wanapumua kwa shida, wanakohoa na kupiga chafya
Uharo wa rangi ya kijivu, njano au kijani na unaonuka
Vifaranga wanaonyesha ulemavu
Kuvimba magoti na kifundo cha mbawa
Kichwa, upanga hugeuka kuwa rangi nyeusi au zambarau
Vifo vya kuku vinaweza kufikia asilimia 20.
Tiba

Yapo madawa mengi aina ya antibiotiki na sulfa ambayo yanaweza kutumika kwa ajili ya tiba na kinga.
Pata ushauri wa daktari.
Kuzuia na Kinga

Utaratibu ulio mzuri zaidi ni kuondoa kuku wote kutoka kwenye shamba/banda ambalo ugonjwa
Umethibitishwa, kupuliza dawa za viuatilifu kabla ya kuingiza vifaranga na kuku wapya Mabanda yote ya kuku yapuliziwe dawa za viuatilifu kabla ya kuingiza kuku wapya.

Kuku wapya watenganishwe na kuchunguzwa kwa muda wa angalau mwezi mmoja kabla ya
Kuwachanganya na kuku wengine.

Vifaranga visichanganywe na kuku wakubwa.
Hakikisha unafuata kanuni za ufugaji bora ili kuku wakue vizuri na wasiathirike
Hayo apo juu ni magonjwa ya kuku ambayo huwa yanajitokeza mara nyingi(common) katika mazingira yetu ya nchi lakini yapo magonjwa mengine ambayo sijayataja katika Makala hii kwasababu huwa hayajitokezi mara nyingi katika nchi yetu. Zifuatizo ni njia kuu za jumla za kuzuia magonjwa ya kuku.

Kutunza hali ya usafi ndani ya banda na kudhiditi kusiwe na unyevu
Matandazo yakichafuka yabadilishwe
Vyombo vya maji visafishwe kila siku
Jitahidi uepuke kufuga kwa njia ya huria ili kuku wako wasiambukizwe magonjwa kirahisi
Epuka kufuga kuku wako pamoja na bata na khanga. Hawa ni wabebaji wa vimelea vya magonjwa ya kuku japo wao hubaki salama
Zingatia ratiba za chanjo kwa magonja yasiyo na tiba kama kideri na mengineyo yanayosababishwa na virusi
Makala hii Imeandaliwa na:

John Mabena,

Mtaalamu wa Sayansi ya Wanyama aliyehitimu katika Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA)

Namba: +255 756 932 721

Barua Pepe: sijalimabena@gmail.com

Leave a Reply