UFUGAJI BORA WA SUNGURA

UFUGAJI BORA WA SUNGURA

SEHEMU YA KWANZA.

UTANGULIZI

Ufugaji wa sungura ni moja wapo ya chanzo kizuri cha mapato nchini Tanzania kama watanzania watafanya yafuatayo,

 • Mfugaji anatakiwa awe na shauku na dhamira ya kweli ya ufugaji.
 • Kufanya tathmini ya rasilimali alizonazo kwa ajili ya mradi wa ufugaji wa sungura.
 • Chanzo endelevu cha mtaji kwa ajili ya mradi.
 • Hulka ya uvumilivu na kuthubutu.
 • Malengo thabiti ya ufugaji wa sungura.
 • Tathmini ya soko la bidhaa za sungura.
 • kujipatia maarifa ya msingi ya ufugaji wa sungura

 

Hivyo Kabla hujaamua kufuga sungura unatakiwa hakikisha ya kwamba umejitoa na una muda wa kuwahudumia wanyama kwani sungura wanahitaji uangalizi na hasa kwenye usafi kwa sababu ni rahisi kwao kupata maradhi yatokanayo na mazingira mabaya na machafu.

 

FAIDA ZA UFUGAJI WA SUNGURA

 • Uzalishaji wa nyama
 • Chanzo cha mapato
 • Huzalisha ngozi kwa ajili ya shughuli mbalimbali za binadamu kama vile kutengeneza viatu.
 • Huzalisha mbolea kwa ajili ya matumizi ya shambani  Mkojo wa sungura hutumika kutengeneza mbolea.
 • Sungura huweza kutumika kwa ajili ya maonesho

 

MAMBO YA MSINGI YA KUZINGATIA KABLA YA KUANZA SHUGHULI YA UFUGAJI WA SUNGURA.

Kitaalam mtu yeyote anaepanga kuanzisha mradi wa ufugaji wa sungura anatakiwa kuwa makini na mambo yafuatayo;

1.Aina ya sungura.

Kufahamu aina ya sungura anayotaka kufuga na yenye kuendana na mazingira anayoishi maana kuna aina nyingi za sungura wafugwao duniani.

2. Hali ya hewa ya eneo unalotaka kufugia.

Hapa tunaangalia zaidi katika unyevunyevu na joto katika eneo husika. Hivyo sehemu nzuri kwa ajili ya kuzalishia sungura ni sehemu yenye joto la wastani 26oC-27oC ambayo itawafanya wakue kwa afya njema.

3. Lishe

Suala la lishe linachukua asilimia 70-80 katika ukuaji wa sungura Hivyo ulishaji wa chakula bora kwa sungura huleta mabadiliko makubwa katika ukuaji wao na lishe mbaya huwafanya kutokuwa na afya bora na ukuaji wao huzorota.Sungura hupendelea zaidi majani na chakula cha kuchanganya kwa kuzingatia mahitaji yao.

 

4.Magonjwa

Kama walivyo wanyama wengine sungura nao hushambuliwa na magonjwa pamoja na viroboto ambayo husababisha kuzorota kwa ukuaji wa sungura na inaweza kusababisha hadi kifo. Mfano wa magonjwa ambayo mara kwa mara huwasumbua sungura ni koksidiosis, “enteritis” na

“pasteurellosis”.

5. Ufahamu juu ya ufugaji wa sungura.

Ufugaji wa sungura una taratibu zake na zinatakiwa kufuatwa ili kuw ana matokeo bora katika shughuli yote ya ufugaji wa sungura. Hivyo mfugaji anatakiwa kufahamu mbinu zote kuanzia anapomleta sungura bandani mpaka anapoenda kumuuza.

Ni matumaini yangu kuwa wewe mfugaji mtarajiwa hata wewe ambaye tayari umeshaanza kufuga umeweza kufaidika na kujifunza mbinu muhimu unazopaswa kuzitambua kabla ya kuanza mradi wa kufuga sungura, ukiweza kuzizingatia mbinu hizo utaweza kujikomboa wewe na familia yako lakini pia utawakomboa watanzania katika suala la ajira. Usikose kuungana na mwandishi wa makala hii katika sehemu ya pili ambayo itazungumzia “Aina za sungura wanaofaa kufugwa Tanzania pamoja na maeneo sahihi kwa ajili ya ufugaji wa sungura”. Kwa mawasiliano zaidi kuhusu masuala yote yanayohusiana na ufugaji wa sungura;

Lucas Joseph

Extension Officer ITL

0655742404/0785403023

Lucas.joseph376@gmail.com

Leave a Reply