ZIJUE MBOLEA ZA ASILI NA MATUMIZI YAKE KATIKA KILIMO.

UTANGULIZI.

Mbolea ni chakula cha mimea ambacho ni mchanganyiko wa virutubisho mbalimbali vinavyoongezwa kwenye udongo au vinavyowekwa moja kwa moja kwenye mimea ,ili kuongeza ukuaji na uzalishaji wa mimea.Kuna aina mbili za Mbolea nazo ni:(a) Mbolea za asili (b)Mbolea za viwandani(Kemikali).

Mbolea za asili hufaa Zaidi kutumika wakati wa kuandaa shamba kabla ya kupanda mazao shambani ambapo mkulima anapaswa kuchanganya mbolea hiyo na udongo wakati wa kulima kabla ya kupanda mazao shambani.

Mbolea za asili huwa na virutubisho vya kutosha vya NPK yaani Nitrojeni,Fosforasi na Potasiumu.Na virutubisho vyote ni muhimu katika udongo na kwa mazao pia.Zifuatazo ni aina za mbolea za asili;

►Samadi.

Hii ni aina ya mbolea ya asili ambayo hutokana na vinyesi vya wanyama kama ng’ombe,kuku,mbuzi,kondoo na wengine. Hii ni miongoni mwa mbolea ambazo wakulima wengi wanaweza kumudu kirahisi. Mbolea ya samadi ni mbolea yenye manufaa zaidi kwani wataalamu wanakadiria kuwa tani moja ya vinyesi vya fahali (madume ya ng’ombe) huwa na thamani karibu kilo 6.3 za chumvichumvi za nitrates; tani moja ya samadi ya vinyesi vya ng’ombe majike huwa na kilo 5.1 za chumvi za nitrates.

Hivyo samadi yenye mchanganyiko wa vinyesi vya ng’ombe majike na madume wanaofugwa kwa pamoja (wanaolala katika zizi moja) huwa na thamani kubwa.

Ili upate kustawi na kutoa mavuno mengi na bora, mimea huhitaji chumvichumvi za madini ya nitrates, phosphate na potash pamoja na kiasi kidogo sana cha chumvi za nitrates, phosphate na potash pamoja na madini ya boron, copper, manganese, zinc na nyinginezo.

Kwa hiyo rutuba ya udongo huwa inategemea sana kiasi cha chumvichumvi zilizomo udongoni.
Ubora wa samadi hukadiriwa pia kwa kiasi cha chumvi za madini zinazopatikana mathalani ng’ombe 50 wanaweza kutoa karibu tani 600 za samadi kila mwaka. Kiasi hiki cha samadi kinaweza kurejesha ardhini karibu kilo 3048 za chumvichumvi za nitrates, kilo 544 za phosphate na kilo 2722 za Potash, pamoja na kiasi kidogo cha Boron, Copper, Manganese na Zinc.

Wakulima au wafugaji wengi hufuga ng’ombe hata zaidi ya 50, lakini kwa wastani wengi huwa na idadi hiyo kama ni wastani wa ng’ombe ambao kila mkulima anaweza kuwa nao.

Mbolea yenye kilo 3048 za nitrates, kilo 544 za phosphate na kilo 2722 za potash kwa uwiano huo haziwezi kutengenezwa kiwandani kwani itakuwa ghali sana kiasi kwamba hakuna mkulima anaweza kununua.

Samadi kiasi hicho italeta manufaa mengi kwani licha ya kuongeza rutuba ardhini vilevile itaubadili udongo uwe katika hali nzuri zaidi kwa kustawisha mimea.

Kadhalika samadi unaufanya udongo ushikamane kwa nguvu zaidi hata usiweze kupeperushwa na upepo au kumomonyolewa na maji ya mvua.

Manufaa mengine ya mbolea ya samadi ni kuwa inaufanya udongo kuwa katika hali nzuri ya kuweza kuyashikilia maji au unyevu kwa muda mrefu.

Minyoo waishio udongoni ambao husababisha kuwepo nafasi kwa ajili ya hewa kupenya kwa urahisi na vijidudu vya bakteria ambavyo huozesha mbolea na kubadili hewa kuwa katika hali ya chumvichumvi zinazotumiwa na mimea, hupata mazingira mazuri kwa maisha yao katika udongo uliotiwa samadi.

Wataalamu wanasema kuwa ubora wa samadi inategemea jinsi ilivyokuwa imetunzwa zizini au kibandani kwani chumvi nyingi hasa zile za nitrates huwa zinapotea kwa urahisi kwa maji ya mvua, kutokana na kitendo chake cha kuyeyuka mara tu zinapolowa maji.

Ili tuendelee kuwa na thamadi kubwa ni muhimu zizi liwe na paa lisilovuja kusudi maji ya mvua yasilowanishe, la sivyo ng’ombe wafugwe katika vibanda.

Samadi hutumika Tani 4 katika shamba la Ekari moja ambalo linakuwa na eneo la mraba 400m2 ,hivyo katika shamba la ukubwa wa Hekta moja lenye eneo la mraba 10000m2 ambayo ni sawa na Ekari mbili na nusu samadi hutumika Tani 10.

►Mboji.

Hii pia huitwa Mbolea mbolea hai au mbolea vunde. Mboji ni aina ya mbolea ya asili yenye rangi nyeusi na harufu nzuri ya kidongo ambayo hutokana na kuoza kwa mchanganyiko wa masalia ya mimea kunakosababishwa na vijidudu na wadudu rafiki wa mazao. Mboji ni urutubishaji wa asili ambao hujirudia wenyewe kwa mtindo wa kuoza. Utengenezaji wa  mboji ni njia ya kurudisha rutuba ya asili kwenye udongo kwa njia ya kuozesha vitu.

Matokeo yake ya mwisho ni kutoa mbolea asili ambayo ni rahisi kutengeneza, na ambayo ina virutubisho vingi bila gharama.Mboji huwa ni faida kutokana na uozaji wa asili ambao hutokea kwenye vitu vyote vyenye uhai.

Vitu vyenye uhai ni kama vile majani, miti na mabaki ya vyakula.wakati wa uozaji vitu hivi hugeuka na kuwa rutuba inayorudia kwenye udongo.Udongo hupoteza virutubisho baada ya kutumika sana .

Inaruhusu mmea kupata rutuba kwa urahisi kutoka kwenye udongo. Pia hufanya mmea usiwe dhaifu kwahiyo huzuia wadudu waharibifu kushambulia mmea.

Mboji hutoa virutubisho kwa muda mrefu kwasababu ya uendeleaji wa kuoza polepole. Madini yaliyopo katika mboji husaidia kuyeyusha madini mengine yaliyo kwenye udongo,Pia  hufanya madini yenye rutuba yapatikane zaidi kwa mimea. Madini hayo huimarisha sehemu laini za mizizi na hivyo kuipa mizizi uimara wa kuweza kupata maji na virutubisho kwa njia ya mizizi

►Mbolea ya maji.

Mbolea ya maji hutengenezwa kwa kuchukua kiroba kilichojazwa samadi, aina mbalimbali ya mimea yenye virutubisho na inayoaminika kuwa dawa ya mimea. Kiroba hicho kinafungwa kwenye kijiti, na kutumbukiza kwa kuning’inia kwenye pipa lililojazwa maji.

Kiroba hicho ni lazima kichukue kati ya kilo 30-50 za samadi pamoja na aina nyingine za mimea kwa maji lita 200 (tazama mchoro). Unaweza kushika upande mmoja wa mti na kunyanyua na kushusha kila baada ya siku tano ili kuchanganya na kuharakisha kutolewa kwa virutubisho zaidi.

Kwa kawaida mchanganyiko huo unakuwa na harufu kali sana maana Nitrojeni nyingi inayopatikana hugeuka kuwa Amonia. Ni vizuri kufunika pipa ili kuzuia kuyeyuka kwa nitrojeni. Harufu ikishaisha, ujue mbolea yako ipo tayari kwa matumizi.

Ongeza maji na utingishe vizuri kabla ya kutumia. Nyunyizia mimea yako kila wiki mpaka utakapoona mabadiliko.

Mbolea ya kunyunyiza ni nzuri kwani inasaidia kuupa mmea virutubisho moja kwa moja kupitia kwenye majani au shina ambapo ndipo chakula kinahitajika.

Faida za mbolea ya maji ni pamoja na kuongezeka kwa kiwango cha mavuno, uwezo wa mimea kukabiliana na wadudu pamoja na magonjwa, kuvumilia ukame, na kuongeza ubora wa mazao.

Ili upate matokeo mazuri wakati wa kunyunyiza mbolea ya maji unatakiwa kufuata vigezo vifuatavyo:
• Inashauriwa kutumia mbolea iliyochanganywa vizuri ili kuepukana na kuunguza mimea.
• Acha maji utakayotumia kuchanganyia mbolea yako nje katika pipa lililowazi usiku kucha, hii inasaidia kutoa madini hatarishi, na kufanya mchanganyiko wenye faida kwa mimea.
• Unatakiwa kutingisha vizuri mbolea yako ya maji kabla ya kunyunyiza. Chembechembe ndogo ambazo hazikuyeyuka zinaweza kuziba mdomo wa bomba la kunyunyizia.
• Matokeo mazuri yanaweza kupatikana endapo mbolea imechanganywa vizuri na kunyunyiziwa wakati hakuna upepo.
• Unatakiwa kunyunyizia mbolea wakati wa asubuhi au jioni wakati hakuna joto na upepo ukiwa umepungua.

►Mbolea ya majivu.

Majivu yanakiwango cha wastani wa madini kifuatacho potasiam 5% – 7%, kalsiam 25% – 50%, fosforas 1.5% – 2% na madini mengine kwa kiasi kidogo pia mabaki mabaki ya chenga za mkaa kwenye majivu pia yanasaidia kwenye kunyonya baadhi ya sumu kwenye ardhi, kumbuka mkaa ni kaboni halisi (pure carbon)

Kiasi cha kilo 2.5 mpaka 5 cha majivu kitumike kwenye eneo la mita za mraba 33 au futi 100 za mraba, na majivu yamwagwe wiki 3 – 4 kabla ya kupanda kitu chochote ardhini.

Kila kitu kikitumiwa zaidi ya kiasi kina madhara na majivu pia yana madhara kwenye udongo kwa sababu yana hali ya kuwa alkaline zaidi (10 – 12 pH)  kwa sababu baadhi ya mchanganyiko wake hauyayuki kwenye maji, kama utahitaji kuongezea kwenye mimea yenye upungufu wa madini kama fosforas na potasiam basi hakikisha majivu hayagusi mashina kwani yanaweza kuuungua haya kama mimea ni michanga.

Pia majivu yana kiasi kidogo sana cha naitrojeni ambacho hakiwezi kukidhi mahitaji ya mmea wowote ule, kwa hiyo hakikisha pia unatumia vyanzo vingine kwa ajili ya naitrojeni, vyanzo kama mimea jamii ya mikunde, marejea na alfalfa.

 

 

 

 

 

VIRUTUBISHO.

Virutubisho ni mahitaji ambayo mmea unahitaji katika ukuaji wake mpaka kufika wakati wa mavuno,virutubisho hivi huwa ni madini ambayo kila mmea unayahitaji madini hayo katika ukuaji wake.Virutubisho hupatikana katika udongo lakini sio kila udongo una virutubisho hivyo mkulima huongeza virutubisho kwenye mmea kwa kumua mbolea ambazo zinakuwa na madini mbalimbali mmea unaohitaji na pia virutubisho husaidia kuongeza rutuba katika udongo.

Mimea inahitaji virutubisho kumi na sita ili kukua na kutoa maua na mazao mazuri.Virutubisho hutumika kama lishe ya mimea.

Virutubisho vitatu hutoka hewani mambavyo ni: kaboni, oxijeni na hydrojeni.—Ikichangia asilimia 93 ya mahitaji ya mmea.Wakati virutubisho vitatu hutokana na hewa na maji .

vingine kumi na tatu hupatikani kupitia udongoni.Hupatikana kupitia mizizi na kutumika na mimea.

Matumizi ya rutuba kwenye udongo

 • Mimea huchukua /huondoa virutubisho kutoka kwenye udongo kupitia kwenye mizizi.
 • Virutubisho vinavyotumika na nafaka kama (ngano, mahindi, mpunga, n.k) inageuzwa kuwa punje na sehemu kwenye masalia ya mimea.
 • Kwa upande wa mahindi ,kwa kila kilogramu 1000 ya mazao yanayozalishwa ,Kilogramu 35 za virutubisho zinakuwepo kwenye mazao na kilogramu 37 kwenye masalia  ya mimea.Jumla ya kilogramu 72 za virutubisho zinakuwa zimetoweka.
 • Iwapo kwenye hekta moja umevuna tani 4 =kilogramu 4000, kiasi cha kilogramu 288 ya virutubisho itakuwa imeondolewa kutoka kwenye udongo.
 • Kama hivi virutubisho havitarudishwa, rutuba ya udongo itapungua .Kwa miaka kadha wa kadha, mavuno kutoka kwenye udongo wa aina hiyo inashuka.
 • Kwa udongo kubaki na rutuba, ni vizuri kurudisha virutubisho vilivyo potea wakati wa mavuno ya mazao.

FAIDA ZA MBOLEA ZA ASILI.

 1. Gharama nafuu.

Huhitaji kuwa na mtaji mkubwa wa kifedha ili kupata aina hii ya mbolea lakini kikubwa Zaidi gharama huwepo katika usafirishaji wa mbolea hiyo.

 1. Huongeza ,kujenga na kukuza mpangilio wa udongo.

Mbolea ya asili hufanya hewa kupenya kwenye mchanga na husaidia utoaji maji shambani hasa huzuia mmomonyoko wa udongo shambani.Pia mbolea hii hufanya udongo aina ya mchanga kuwa na maji au unyevunyevu wakati wa kiangazi kwa kutengeneza mpangilio wa mchanga,hufanya mimea kukua kwa urahisi na kukua kwa afya na kutoa mavuno mengi.

 1. Kutunza ubora wa udongo.

Mbolea ya asili hutunza ubora wa udongo kwa kuongeza madini yanayohitajika na mimea,hii husaidia kuongeza mazao ya mimea

 1. Kupunguza wadudu wa mimea walioko kwenye udongo.

Hii husaidia mimea kuwa na nguvu ,afya na hustahimili magonjwa na wadudu waharibifu.

 1. Haibebwi na mvua na kuhamishwa.

Mbolea ya asili haibebwi na mvua kama ilivyo mbolea za kemikali ,hivyo mbolea ya asili huwa na sifa ya kudumu kwa mda mrefu katika shamba.

 1. Kuondoa wadudu rafiki wa mimea.

Hii ni tofauti na mbolea za kemikali ambazo huvutia wadudu waharibifu na kuondoa mazingira rafiki ya wadudu muhimu.

 1. Huupatia mmea virutubisho vingi.

Mbolea za viwandani zina virutubisho baadhi kwa kiasi Fulani Zaidi ya vingine ,lakini mbolea za asili zina utajiri wa virutubisho.

 1. Huwezesha mizizi ya mimea kukua vizuri kuelekea kwenye virutubisho muhimu.

Hii hufanyika kutokana na kuboreshwa kwa muundo wa udongo.Kama udongo ulikuwa ulikuwa umeshikana ,unapoweka mbolea asilia huwa laini ,hivyo kurahisisha mizizi kupenya kwa urahisi.

 1. Kuongeza PH ya udongo.

Moja ya matatizo yanayopunguza uzalishaji ni mkulima kuwa na udongo wenye PH ya chini dhidi ya mazao yake.Kwa kuweka mbolea ya asili PH huongezeka hivyo kuuweka mmea katika hali nzuri ya kuongeza uzalishaji.

HASARA ZA MBOLEA YA ASILI.

 1. Mbolea ya asili haiwezi kuokoa mmea unaokufa.

Hii ni kwa sababu huchukua mda mrefu kuchukuliwa na mmea.Wakati mbolea ya viwandani ikishalowanishwa tu haraka huchukuliwa na mmea.Mbolea ya asili inahitaji kuoza Zaidi na kuvunywavunjwa.

 1. Upatikanaji wake ni mgumu.

Wakulima wengi wanashindwa kupata mbolea ya asili kwa haraka.Hii ni kutokana na wafugaji wa wanyama kama ng’ombe kuwepo maeneo ya mbali.

 1. Huhitajikakwa wingi.

Mbolea hii huitajika kwa wingi Zaidi,mfano;kwa ekari moja mkulima anaweza kuhitsji kuanzia tani12 kwa sababu mbolea ya asili inahitajika kuwekwa wa wingi

 1. Huathiri mmea.

Inawezakukausha mmea mara moja kama itawekwa bila kuzingatia hali ya mbolea hiyo.Kwa mfano ikiwekwa ikiwa haijaoza  vyema inasababisha mmea kuungua na kukauka.Lakini pia ikiwekwa mbichi inaweza sababisha magonjwa ya fangasi na bakteria kwa mmea..

 1. Ni ngumu kujua virutubisho unavoongeza.

Mbolea za kemikali huwa na virutubisho vikuu vitatu kwa ukuaji bora wa mmea wako.Hivyo wakati mkulima anaweka hujua kabisa ni kiwango gani cha nitrojeni,fosiforusi au potasiamu anaweka.Kwa mbolea ya asili mkulima hawezi kujua ameweka kiasi gani cha virutubisho hivyo muhimu

 HITIMISHO.

 • Matumizi ya mbolea za asili nayo ni mazuri katika kuendeleza udongo kwa ajili ya ukulima.
 • Mbolea ni kitu muhimu sana katika udongo kwa sababu mazao huitaji virutubisho katika udongo na baada ya udongo kutumika kwa muda mrefu , virutubisho hupotea.
 • Kuvirudisha virutubisho, mbolea inahitajika inaweza ikawa ya chumvichumvi au ya asili hii hutegemea na udongo uliopo katika sehemu hiyo.
 • Kila sehemu ina udongo wa aina yake na unahitaji virutubisho vya aina yake kwa wingi au kiwango kidogo.
 • Kwa hiyo uwekaji wa mbolea katika udongo lazima utumie utaalamu ambao mkulima amepata kutoka kwa wataalamu wa kilimo au uzoefu

 

 

 

Imeandaliwa na; ADRIA NOLASCO PANCLAS.

Mawasiliano      ; +255 653 827 565.

Barua pepe        ; adria.nolasco24@gmail.com

 

 

 

1 comment on “ZIJUE MBOLEA ZA ASILI NA MATUMIZI YAKE KATIKA KILIMO.

Leave a Reply